1 Timothy 6

Watumwa

1 aWale wote walio chini ya kongwa la utumwa inawapasa kuwahesabu mabwana zao kuwa wanastahili heshima yote, ili jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu. 2 bWale watumwa ambao wana mabwana waaminio, haiwapasi kupunguza heshima yao kwa sababu wao ni ndugu. Badala yake, wawatumikie hata vizuri zaidi, kwa sababu wale wanaonufaika na huduma yao ni waaminio, ambao ni wapenzi wao. Fundisha mambo haya na uwahimize kuyafuata.

Mafundisho Ya Uongo Na Utajiri Wa Kweli

3 cIkiwa mtu yeyote atafundisha mafundisho mapotovu wala hakubaliani na mafundisho manyofu ya Bwana wetu Isa Al-Masihi na yale ya utauwa, 4 dhuyo amejivuna wala hajui kitu chochote. Yeye amejaa tamaa ya mabishano na ugomvi kuhusu maneno ambavyo matokeo yake ni wivu na mapigano, maneno ya ukorofi, shuku mbaya, 5 ena kuzozana kusikokoma kati ya watu walioharibika akili zao, walioikosa kweli, na ambao hudhani kwamba utauwa ni njia ya kupata faida.

6 fLakini utauwa na kuridhika ni faida kubwa. 7 gKwa kuwa hatukuja humu duniani na kitu chochote, wala hatuwezi kutoka humu na kitu. 8 hLakini kama tuna chakula na mavazi, tutaridhika navyo. 9 iLakini wale watu wanaotamani kuwa na mali kwa haraka huanguka kwenye majaribu, na wamenaswa na tamaa nyingi za kipumbavu zenye kudhuru, zinazowazamisha watu katika uharibifu na maangamizi. 10 jKwa maana kupenda fedha ndiyo shina moja la maovu ya kila namna. Baadhi ya watu wakitamani fedha, wameiacha imani na kujichoma wenyewe kwa maumivu mengi.

Vitu Vizuri Vya Imani

11 kLakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole. 12 lPigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi. 13 mNakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai, na mbele za Al-Masihi Isa ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri, 14 nuishike amri hii bila dosari wala lawama mpaka kuja kwake Bwana wetu Isa Al-Masihi, 15 oambaye Mungu atamleta kwa wakati wake mwenyewe: yeye ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana, 16 pyeye peke yake ambaye hapatikani na mauti, na anakaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa, ambaye hakuna mwanadamu aliyemwona wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye milele. Amen.

17 qWaagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. 18 rWaagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali zao na wengine. 19 sKwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani, ule uzima ambao ni wa kweli.

Maelekezo Ya Binafsi Na Maombi Ya Baraka

20 tTimotheo, linda kile kilichowekwa amana kwako. Epuka majadiliano yasiyo ya utauwa na mabishano ambayo kwa uongo huitwa elimu, 21 uambayo wengine kwa kujidai kuwa nayo wameiacha imani.

Neema iwe nanyi. Amen.
Copyright information for SwhKC